HOTUBA YA RAIS KIKWETE - UNFUGUZI FBME ARUSHA


Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA SHEREHE YA UFUNGUZI WA TAWI JIPYA LA BENKI YA FBME, ARUSHA TAREHE 08 SEPTEMBA, 2009

Mwenyeji wetu, Bw. Ayoub Farid Michel Saad, Mwenyekiti FBME Group;
Mheshimiwa Dkt. Deodorous Kamara (Mb), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Isidor Shirima, Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Meneja Mkuu wa Benki ya FBME;
Wakurugenzi wa FBME;
Waageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Asalaamu Aleykum!


Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuja kushiriki katika uzinduzi wa Tawi Jipya la Benki ya FBME katika jiji la Arusha. Jiji ambalo lina sifa nyingi, ni muhimu kwa utalii, ni makao makuu ya mashirika kadhaa ya kikanda na kimataifa yakiwemo Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda na Mahakama ya Afrika ya haki za Watu n.k.

Namshukuru Bwana Ayoub Farid Michel Saad, Mwenyekiti wa FBME Group, na viongozi wa Benki hii kwa kunialika katika sherehe hii. Nafurahi kwamba Benki hii imeimarika vizuri na mtaji wake umeongezeka kiasi cha kuweza kufungua tawi jingine hapa Arusha.


Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama mnavyoelewa fedha ni kichocheo muhimu cha maendeleo. Hivyo basi, ukuaji wa sekta ya huduma za kifedha ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Ili sekta ya fedha iweze kutoa mchango unaokusudiwa, inapaswa iwe imara, na iwe na uwezo mkubwa wa kufikia wateja wengi mijini na vijijini. Benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi. Benki zinatakiwa zizingatie mahitaji ya wananchi na ziweze kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kutumia huduma za benki.

Sekta ya kibenki nchini imekua sana. Hivi sasa kuna jumla ya benki 39 na kati ya hizo 26 ni benki kamili za biashara na kumi na tatu ni taasisi za kifedha. Benki hizo kwa pamoja zina jumla ya matawi 400. Mengi ya matawi haya yakiwa katika jiji la Dar es Salaam. Kati ya benki hizo, 16 zinamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 na nyingine 12 zinamilikiwa na wageni kwa asilimia 100. Taasisi 11 zinamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wawekezaji wa nje.

Ukuaji huu umesaidia kuongezeka kwa mitaji ya benki na kutanuka kwa huduma za kibenki nchini. Rasilimali za benki zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 2,953.84 mwaka 2004 hadi kufikia shilingi bilioni 9,106.40 mwezi Juni 2009. Mikopo iliyotolewa ilifikia shilingi bilioni 4,440.34 mwezi Juni 2009, ikiwa ni ongezeko la asilimia 353 kutoka mwaka 2004. Amana zilizowekwa na wateja katika taasisi za kibenki ziliongezeka kwa asilimia 218 na kufikia shilingi bilioni 7,050.58 na mtaji uliongezeka kufikia shilingi bilioni 1,128.83 sawa na ongezeko la asilimia 292. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa sekta yetu ya kibenki imekua na kutanuka kwa kasi kubwa na inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu. Kukua huku ni habari njema sana. Inaonyesha imani kubwa iliyokuwepo kwa sera za uchumi na siasa za Tanzania.

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Mafanikio haya makubwa ya sekta ya benki nchini yanajumuisha pia mchango wa Benki ya FBME. Mpaka sasa benki hii ina matawi manne katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Zanzíbar na Arusha. Nimefahamishwa kuwa matawi mengine mawili yapo nchini Cyprus na wanayo pia ofisi ya uwakilishi mjini Moscow, Urusi. Nimefahamishwa pia kuwa benki hii ni ya kwanza kati ya benki zenye makao makuu yake hapa nchini kuwa na matawi yake nje ya Tanzania.

Napenda kuwapongeza viongozi na watumishi wa benki FBME kwa mafanikio makubwa ambayo benki yenu imepata tangu ilipoanzishwa mwaka 2003. Nimefahamishwa kwamba kufikia tarehe 30 Juni 2009 benki hii imekuwa na rasilimali zenye thamani ya shilingi bilioni 202.78 kutoka shilingi bilioni 55.35 mwaka 2004. Hili ni ongezeko la asilimia 266. Benki hii pia imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 121.99 na amana zilizowekwa na wateja zimefikia shilingi bilioni 131.27. Hongereni sana!

Nawapongeza na kuwashukuru ndugu zetu wa FBME kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo. Nimefurahishwa kusikia kuwa asilimia 17 ya mikopo yenu imetolewa kuendeleza shughuli za kilimo. Hiki ni kielelezo wazi cha kuunga kwenu mkono juhudi za Serikali za kuleta mapinduzi ya kilimo. Naomba muendelee kuwa na msimamo huo, hasa kwa sasa, kwa kuunga mkono mkakati wetu mpya wa kilimo maarufu kwa Kilimo Kwanza. Wakati nawaomba muendelee kuwa na moyo huo, pia napenda kuziomba benki nyingine zifanye hivyo hivyo, kwani Serikali inahitaji sana washiriki wa kibenki kama nyinyi katika kufanikisha mpango wa kuleta mageuzi katika kilimo.


Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Pamoja na mafanikio haya natambua kuwa sekta ya fedha inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinahitajika kushughulikiwa ili kuhakikisha kuwa huduma ya fedha inatolewa kwa ufanisi na urahisi ili iweze kuwafikia na kuwahudumia watu wengi zaidi mijini na vijijini. Takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 9 tu ya Watanzania wote ndio ambao wanapata huduma za benki. Asilimia 2 wanapata huduma za kifedha kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOs) na taasisi zingine za fedha. Asilimia 35 ya Watanzania wanapata huduma kupitia njia zisizo rasmi na asilimia 54 ya Watanzania waliosalia hawapati huduma za fedha. Hii ni idadi kubwa mno ambayo haifai kuachwa hivyo. Hali hii inazitaka Benki zibuni mikakati na mbinu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma za kibenki. Aidha, natoa wito kwa Watanzania wenzangu wote kujenga mazoea ya kuweka akiba zao benki na kutumia benki kwa shughuli zao za kifedha.


Kama nilivyosema wakati nafungua Benki ya Wanawake Tanzania, napenda kurudia tena hapa kutaka pawepo na mpango wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia benki kuweka akiba na kufanyia shughuli za malipo. Wananchi waelimishwe kwamba, wakiwa na akaunti benki pesa zao zinakuwa salama na wakifanya malipo kupitia benki wanajijengea historia nzuri ya kukopesheka. Kufanya hivyo kunafanya iwe rahisi kupata mikopo kutoka benki kwani huwa ngumu kwa wale ambao si wateja wa benki.


Changamoto nyingine ninayopenda kuizungumzia ni riba kubwa inayotozwa kwa mikopo ya benki. Kwa kweli inakatisha tamaa watu kukopa hivyo benki hazina budi kuangalia upya sula hili. Natambua kuwepo tatizo la baadhi ya wakopeshwaji kutorejesha mikopo na kesi zinazohusu mabenki kuchelewa kuamuliwa Mahakamani ni sababu mojawapo zinazosababisha riba kuwa juu. Sijui kama wenye benki wametazama sababu za watu kushindwa kulipa na kubaini kwa kiasi gani riba kubwa imechangia hali hiyo. Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imefanikiwa kupunguza riba ya hatifungani ya Serikali. Moja ya shabaha ya kufanya hivyo ni kutaka riba za mabenki zipungue. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama imekuwa inachukua hatua mbalimbali za kuongeza ufanisi katika Mahakama zetu nchini hususan ili kuongeza kwa kasi ya kushughulikia na kumaliza mashauri yaliyoko mahakamani. Kuundwa kwa Mahakama ya Biashara ya Mahakama Kuu, kuongeza idadi ya Majaji na kuboresha vitendea kazi ni miongoni mwa hatua hizo. Naomba mabenki yaunge mkono jitihada hizo za Serikali kwa kukamilisha mchakato wa uanzishaji wa Credit Reference Bureau pamoja na, hatimaye, kupunguza riba zinazotozwa hasa kwenye mikopo ya biashara ndogo na watu binafsi.


Mheshimiwa Waziri;
Kuendelea kupanua wigo wa huduma ambazo zinatolewa na benki kukidhi mahitaji mbalimbali ya uchumi unaokua ni jambo linalohitaji kushughulikiwa vizuri. Serikali imetunga Sheria ya Ukopeshaji Vifaa (Leasing Finance) pamoja na kuboresha Sheria ya Mikopo ya Nyumba (Mortgage Finance). Vilevile, Serikali imechukua hatua za kuwawezesha wanavijiji kupata hati za kumiliki mashamba yao kimila na hati hizo kuweza kutumika kukopa benki. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba Serikali inaimarisha mazingira ya utoaji wa huduma za kifedha. Nayasihi mabenki kutuunga mkono katika kufanikisha hili. Nafurahi kusikia benki ya FBME imeanza utaratibu wa ukopeshaji wa zana za kilimo kule Morogoro. Endelezeni huduma hiyo kote nchini. Naomba mabenki mengine yafanye hivyo.


Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Mwisho napenda kumaliza kwa kuyaomba mabenki kuzingatia sheria za nchi katika kutekeleza majukumu yao. Aidha, taasisi zinazosimamia shughuli za kibenki hazina budi kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuepuka madhara yanayoweza kuwakumba wateja kutokana na kufilisika kwa benki.

Baada ya kusema maneno hayo mengi, sasa napenda kufanya kile kilichotukusanya hapa leo hivyo kwa heshima na taadhima natamka kuwa, Tawi la Benki ya FBME Arusha limefunguliwa rasmi.


Mungu Ibariki Afrika! Mungu ibariki Tanzania!

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Postagem Anterior Próxima Postagem